JULIO: ‘ WATANZANIA WASIINGILIE KAZI ZA MUNGU, CHUJI NI KIUNGO BORA, MWADUI FC INAKUJA LIGI KUU BARA’
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Jamhuri Kiwhelo ' Julio' ni mchezaji-kocha wa zamani wa klabu ya Simba SC ambaye kwa sasa anaifunza timu ya daraja la kwanza ya Mwadui FC ya Kahama, Shinyanga amefunguka na kusema kuwa ligi hiyo ni ngumu ' kuliko' lakini atahakikisha anaisaidia timu yake kupanda daraja na kucheza ligi kuu. Mwadui wanaongoza moja ya makundi mawili ya ligi hiyo na kila kundi litatoa washindi wawili wa juu kucheza ligi kuu msimu ujao.
" Ligi daraja la kwanza ni ngumu, tena ni ngumu kweli kweli. Ugumu wae ni namna tulivyofungana kwa pointi katika nafasi za juu. Mwadui FC inaongoza ligi ikiwa pointi 22 sawa na Toto Africans, wakati JKT Oljoro aliye katika nafasi ya tatu amekusanya pointi 20 na kwa karibu wapo Polisi Mara wenye pointi 19. Katika hali hiyo ukiteleza kidogo tu unakwenda chini." anasema, Julio.
Mwadui imekusanya wachezaji wengi wenye uzoefu katika kikosi chake na hilo limekuwa ni moja ya sababu ya timu hiyo kufanya vizuri hadi sasa.
" Kwa uimara na ubora wa timu yangu naamini nitapambana kuhakisha tunapanda ligi kuu. Kikubwa kilichotusaidia hadi sasa, kwanza ni uzoefu. Mtazame mchezaji kama, Athuthumani Iddi ' Chuji', hadi sasa ninasikitika sana kuona kwa nini Yanga walimuacha mchezaji kama Chuji. Suala la nidhamu, kusema kweli wachezaji wote ulimwenguni hawana nidhamu, lakini ni jinsi gani unaweza kumtumia mchezaji wa namna hiyo ni kutazama kama kweli anafanya vizuri kazi ya watu. Kama mchezaji hafanyi mambo mabaya wamuachie tu acheze mpira."
" Chuji ni mmoja wa viungo bora ambao wamesaidia sana kuifikisha timu yangu katika nafasi hiyo. Si yeye tu, yuko Said Sued mchezaji mwenye uzoefu mkubwa, Juma Jabu, Julius Mrope, Samuel Ngassa wote hawa wameshacheza ligi ya juu ya Tanzania hivyo wanaposhuka chini kucheza na vijana ambao wanatafuta promosheni ni lazima wakwae ' kigingi' kutokana na uwezo mkubwa wa vijana wangu kiuzoefu, kifundi na kiakili Timu nyingine pia ni nzuri, zinacheza vizuri hasa wanapocheza na timu yangu ( Mwadui) huwa wanakamia kwa kujua wanacheza na ' timu ya Julio'"
Ligi hiyo imesimama kwa muda na kila timu inajipanga kuongeza nguvu katika vikosi vyao wakati huu wa usajili wa dirisha dogo. Julio anasema hatasita kuwasaini wachezaji watakaotemwa na klabu za ligi kuu wakati huu kama watakuwa wenye uwezo kama ilivyo kwa kina Chuji.
" Nasubiri ' mizoga ' ( wachezaji ambao huachwa na timu kubwa nchini), Simba, Yanga, Mtibwa kama wataacha baadhi ya wachezaji wao ambao najua watanisaidia nitawachukua. Watanzania wanisubiri katika ligi kuu. Napenda kuwaambia kuwa wasiingilie kazi za Mungu, kwa sababu hata mwenyezi Mungu kazi nyingine amezikataa, kama kazi ya kuua kampa Israel, sasa kuna watu wanaingilia kazi za mwenyezi Mungu anampa Mtu alafu wao wanataka wanyang'anye, wamuache Mungu afanya kazi zake"
Comments
Post a Comment